Vijana wa Kamishina wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Suleiman Kova kwa kushirikiana na Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers wamefanikiwa kulifumua danguro linalodaiwa kufuga madenti wa vyuo mbalimbali jijini Dar.
KERO
Awali kikosi kazi cha OFM kilipokea malalamiko kutoka kwa wazazi waishio maeneo hayo wakilalamikia ufuska wa kutisha unaofanyika kwenye danguro hilo.
Mzazi:Halooo…nazungumza na OFM?
OFM: Ndiyo…tukusaidie nini?
Mzazi: Mna habari?
OFM: Tunazo nyingi lakini ukitupatia ya kwako tutaifanyia kazi ipasavyo.
Mzazi: Tunawaamini OFM mnatisha kama njaa. Sisi ni wazazi wa hapa Buguruni-Sokoni. Kuna danguro hapa kwa kweli yanayofanyika ni aibu tupu. Tunaomba mje mjionee wenyewe mfanye kazi yenu.
OFM: Nini hasa kinafanyika?
Mzazi: Yaani vitendo vya ngono vinafanyika na sasa hivi hata kwa nje wapo watu wanafanya biashara haramu ya ngono hivyo watoto wetu wanashuhudia vitu vya ajabu na kondomu zimezagaa kila kona.
OFM: Sawa, tuachie tufanye kazi yetu.
Mzazi: Oke, lakini naomba chondechonde msinitaje wala kuonesha namba yangu kwa sababu hii ni biashara ya watu nitamwagiwa tindikali bure!
OFM: Tunaheshimu vyanzo vyetu hatuwezi kukutaja popote kwani siyo maadili ya kazi yetu.
OFM KAZINI
Kabla ya kuwataarifu polisi juu ya kero hiyo kwa wakazi wa eneo hilo, vijana wa OFM waliingia kazini ili kujikusanyia ushahidi ambapo walipofika walishuhudia vitendo hivyo vikifanyika mchana kweupe bila kujali kama kuna serikali.
Baadhi ya makachero wa OFM walijifanya wauzaji na wengine wanunuaji ambapo walijikusanyia data za kutosha huku wakiwarekodi wahusika (madenti wanaojiuza na wanaume wanaowanunua) kwa kutumia vifaa vya kazi bila wao kushtuka.
BEI
Kuhusu bei, wapo wa bei chee kuanzia buku mbili hadi tano na wa bei mbaya ambao siyo wengi, wao wakianzia dau la elfu kumi na kuendelea.
Mmoja wa vijana hao wa OFM alifanikiwa kuingia ndani baada ya kukubaliana bei na mmoja wa wauzaji ambapo alipofika na kujionea mazingira halisi aliahirisha kwa kigezo kuwa alikuwa amepokea simu ya dharura.
USHUHUDA MBAYA
Hata hivyo, alichokishuhudia ndani, anasimulia: “Nilishuhudia watu wakiwa kwenye ‘pea’ wakijiachia kwa ngono na suala la kondom ilikuwa ni uamuzi wa mtu.
“Kondom zilizotumika zilikuwa zimezagaa kila kona yaani nilihisi mwili kunisisimka na kuwaza sana juu ya janga la Ukimwi. Kwa hali ile tumekwisha.”
TAARIFA POLISI
Ili kufanikisha zoezi la kulifumua danguro hilo, OFM iliwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi na kumweleza mchezo mzima wa uchafu unaofanyika eneo hilo.
Bila kusita, kamanda huyo aliteua vijana wake kutoka Kituo Cha Buguruni ambao walitekeleza kwa kiwango cha oparesheni hiyo maalum.
Walipofika eneo la tukio, polisi hao waliwakamata wahusika wote akiwemo mmiliki wa biashara hiyo.
DENTI IFM
Wakati watuhumiwa hao wakihenyeshwa na polisi, mmoja wa madenti hao anayesoma Chuo cha IFM, Peter Davis alisema kwa upande wake aliamua kuweka makazi yake ndani ya chumba kimoja cha danguro hilo
Katika utetezi wake, denti huyo alidai kuwa aliamua kuishi hapo kwa kuwa mazingira hayo ni mazuri kwake kwa ajili ya kujisomea.
Mwingine aliyenaswa ndani ya kiwanja hicho cha maasi ni denti aliyejitambulisha kwa jina la Mwanahamisi (hakutaja chuo) ambaye alidai kuwa tangu siku hiyo atauacha uchangudoa na kuapa kuwa akiachiwa huru ataenda kusoma kwa bidii.
Denti mwingine aliyekamatwa katika msala huo alijitambulisha kwa jina moja la Angel ambaye alidai kuwa anasoma chuo kimoja kilichopo Kariakoo, Dar na wengine hawakutaja majina zaidi ya kukiri kuwa ni wanafunzi.
MUUZA KONDOM NAYE MBARONI
Ndani ya gesti hiyo pia alinaswa njemba mmoja aliyekuwa ameweka maskani na kazi yake kubwa ilikuwa kuuza kondom kwa madenti hao ambao humwingizia kipato chapuchapu.
Hata hivyo, jamaa huyo alitiwa mbaroni kwa uchunguzi zaidi.
Mbali na oparesheni hiyo, pia polisi hao waliendeleza msako maeneo mengine ya Buguruni ambapo dadapoa kibao walikamatwa huku mmoja akiangua kilio na kutamani kujiua kuliko mumewe kujua kuwa anauza mwili.
NYUMA YA NONDO
Baada ya kuhojiwa kuhusika na biashara haramu ya ngono na kukiri, watuhumiwa hao wote waliwekwa nyuma ya nondo kwenye Kituo cha Polisi cha Buguruni na kufunguliwa jalada la kesi namba BUG/RB/13114/2013 - UMALAYA, wakisubiri sheria kuchukua mkondo wake.
WAZAZI SOMENI HAPA
Uchunguzi wa gazeti hili ulionesha kuwa madenti hao na wengine wengi jijini Dar, wamekuwa wakiaga kwao kuwa wanakwenda masomoni lakini kumbe wanaishia kwenye madanguro yaliyojazana jijini kwa ajili ya kujiuza.
Huku wazazi wakitoa fedha nyingi na huduma nyingine wakiamini watoto wao wanasoma, hali ni tofauti kwani madenti wengi wamekuwa wakiishia kwenye vitendo vya kihuni na kufeli masomo na maisha kwa jumla kisha kugeuka mzigo kwa familia.
Gazeti hili linawataka wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao wanaowasomesha ili kuwakanya juu ya kujiingiza kwenye uhuni ambao huhatarisha maisha yao
SOURCE -GPL