Hatimaye serikali imelibomoa eneo lililogeuzwa kuwa danguro la wazi, ambako vitendo vya ngono vilikuwa vinafanyika hadharani, Mbagala Zekhem, jijini Dar es Salaam.
Bomoa bomoa hiyo ilifanywa juzi na Manispaa ya Temeke kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya gazeti hili kuandika habari ya kiuchunguzi ambayo ilibaini watu wa rika mbalimbali kujihusisha na biashara ya ngono ya wazi katika eneo hilo. Eneo hilo lililopo Mbagala Zakhem, limekuwa maarufu baada ya watu kuugeuza uwanja uliojengwa vibanda vya mbao kwa ajili ya biashara ya chakula, kuwa kama eneo huru la kufanyia vitendo vya ngono.
Katika kuonyesha kuwapo idadi kubwa ya wanaoshiriki kwenye biashara hiyo, kila sikuinaelezwa kukusanywa ndoo tatu ya mipira ya kiume (kondomu) iliyotumika.
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo, wameliambia NIPASHE Jumamosi kwamba bomoabomoa hiyo ilifanyika juzi saa 7:30 mchana kwa kutumia magari mawili aina ya kijiko huku polisi wakiweka ulinzi mkali.
"Kila mtu hakufahamu kama wangekuja hawa jamaa kubomoa sehemu hii, tuliona magari na polisi yakivamia na kuanza kubomoa," alisema Abdallah Saidi.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema, alisema amekerwa na vitendo vya kinyama vinavyofanywa na watu hao, hivyo ameamua kupambana nao.
Alisema aliposikia kwamba kuna watu wanafanya ngono hadharani kwa makundi aliumia sana, kwani miongoni mwao wapo watoto. "Haingii akilini kuona watu wazima wanafanya mapenzi hadharani, ni jambo baya na linaharibu watoto wetu ni lazima kuchukua hatua kali," alisema.
Alisema tayari wamebaini kuwapo na madanguro mengine ya aina hiyo (hakuyajataja), kinachofanyika ni kuwa yanafuatiliwa kwa makini, kisha hatua zichukuliwe kuyatokomeza.
"Ukiachana na kukerwa kwangu, pia kwa sasa tupo kwenye zoezi la kusafisha jiji, hatutakubali kuona eneo la wazi linachafuliwa," alisema.
Hata hivyo, Mjema aliwataka wajumbe wa Bunge maalum la katiba mpya, kuhakikisha wanatunga sheria ya ngono ambayo itapiga vita vitendo vya aina hiyo pamoja na ushoga.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Kiondo, alisema kazi wanayofanya ni kusimamia sheria na sio kuwakamata watu wanaojihusisha na biashara hiyo. Alisema kazi ya kupambana na biashara ya ngono inatakiwa uangalifu wa hali ya juu ili kuifanikisha.
Awali mwandishi wa gazeti hili alishuhudia jinsi idadi kubwa ya wanaume wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 50 wenye hadhi tofauti, wakipigana vikumbo kwa kuingia na kutoka kwa ajili ya kupata huduma hiyo chafu.
Aidha, uchunguzi ulibaini kuwa mwanamke mmoja alikuwa akishiriki vitendo vya ngono na wanaume zaidi ya 20 kwa malipo ya Sh. 3000 kwa mkupuo mmoja. Awali, eneo hilo wazi lenye ukubwa kama mita 25, watu walikuwa wakifanya ngono ya wazi huku wanaume wengine wakiwa wamejipanga wakisubiri wenzao kumaliza ili na wao wajinafasi.
Mmoja wa wanawake hao (Jina linahifadhiwa) alisema wapo wanawake zaidi ya 30 na wana uwezo wa kuwahudumia wanaume kati ya 100 hadi 300, hivyo inakuwa kazi ngumu kutumia eneo dogo kwa sababu itawapotezea muda.
WANANCHI WASHANGILIA
Baadhi ya wananchi waliokutwa katika eneo hilo, wamesema wamefurahishwa na hatua hiyo kwa sababu watoto wao walikuwa wakiharibiwa. Walisema walikuwa wakipata taabu kuwaangalia watoto wao kutokana na baadhi yao kubainika huenda eneo hilo.
Christopher Mtandi (25) alisikika akilipongeza gazeti la NIPASHE kwa kuanika uchafu huo na kueleza kuwa hatua hiyo imesababisha serikali kufahamu na kuchukua hatua.
"Kila siku ikifika majira ya jioni eneo lote hili linajaa mipira ya kondomu, sasa tutapumzika kuona uchafu ule ukiendelea," alisema. Naye Amina Mwenyimvua alisema wanaume wengine waliokuwa wakishiriki vitendo hivyo walikuwa na umri chini ya miaka 18.
"Vijana wengi hapa Mbagala wamekwenda eneo lile kupata huduma ya mapenzi, hatujui athari itakayotokea kwani nina uhakika wengi hawajui mbinu ya kujikinga na Ukimwi," alisema Amina.