Polisi mjini Musoma wametumia mabomu ya machozi kudhibiti ghasia zilizoibuka, baada ya wafuasi wa Chadema kupambana na mbunge wa zamani wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo.
Walifanya
fujo juzi jioni baada ya mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC)
kudaiwa kuingilia safari ya Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willbroad Slaa ya
kwenda kwenye msiba wa Sheikh wa Mkoa wa Mara Athumani Mageyee.
Kiongozi huyo alikwenda kuhani msiba wa Sheikh huyo aliyefariki wiki hii.
Hata
hivyo, kabla ya kufika msibani, Mathayo alijitokeza kuelekea nyumbani
kwa Sheikh huyo na kuwalazimisha wafuasi wa Chadema waliokuwa
wameusindikiza msafara wa Dk. Slaa, kupanga mawe barabarani kumtaka
asubiri.
Wakizungumza
kwa jazba wakiwa wanapanga mawe hayo, walisema mbunge huyo wa zamani ni
mwenyeji wa Musoma lakini tangu msiba utokee hajawahi kuhani lakini
alipoona viongozi wa Chadema wanakwenda naye akajitokeza.
“Tunashangaa
huyu Mathayo kuja kwenye msiba baada ya kuona viongozi wa Chadema
wanakwenda wakati yeye ni mwenyeji na hajawahi kukanyaga, sisi tunaamini
hakuwa na lengo zuri na ndiyo tukamzuia,” alisema Jacob Mwita.
Ghasia
hizo zilisababia polisi kulifika eneo la vurumai na kuwatawanya kwa
kupiga mabomu ya machozi, hali hiyo ilidumu kwa muda wa nusu saa na
kusababisha baadhi ya wafuasi wa Chadema kuwashambulia polisi.
Kufuatia
hali hiyo, Mbunge wa sasa wa Jimbo hilo, Vincent Nyerere , alilazimika
kuingilia kati kuwatuliza wafuasi wa Chadema waliokuwa wanaendelea
kupambana na polisi.
CHANZO: NIPASHE