Je
wewe ni mtu wa kupenda ghafla, yaani mwanaume anapokutamkia kwamba anakupenda
huwa unamuamini kwa kiasi gani, unakuwa ni mwepesi wa kumuamini na kujitoa kwa
ajili yake au unakuwa na kujivuta vuta ili kujiridhisha kabla ya kuingia katika
uhusiano? Hebu fikiri kabla ya kuamua, jipe muda kwani hakuna jambo lililo jema
kama subira linapokuja swala la kupenda. Subira itakuepusha
kupoteza muda wako katika mahusiano ambayo hayana mashiko wakati dhamira yako
ilikuwa ni kumpata mwenzi mwenye sifa muafaka, pale utakapoingia mahali ambapo
sipo. Kwa kawaida kutoka katika uhusiano huo kuna gharama kubwa na kunaweza
kukusababishia matatizo mengi yakiwemo ya kiafya.
Hapa
chini nitajaribu kueleza makosa kadhaa ambayo wanayafanya wanawake linapokuja
swal la kupenda:
1.Kumbadili
mtu awe vile utakavyo:
Usije
ukajidanganya kwamba unaweza kumbadilisha mtu mzima na akili zake. Kama umepata
mwanaume ambaye kwa mtazamo wako unamuona ana sifa muafaka lakini anatabia
ambazo huzipendi kwa mfano ulevi au kuvuta sigara vitu ambavyo vinakukera sana,
usije ukajidanganya kwamba unaweza kumbadilisha na akaacha tabia hizo, anaweza
kuacha kwa muda tu ili kukuvuta ukiingia kingi imekula kwako, tabia hiyo
inaweza kujirudia. Ni vyema kama kuna tabia ambazo umezipenda lakini zipo
ambazo huzipendi kutoka kwa mwenzi wako, basi weka uzingativu kwenye zile tabia
unazozipendfa na zile usizozipenda achana nazo, kama ataamua mwenyewe kuziacha
sawa lakini kama akiamua kuendelea nazo, basi zisikuumize kwani unaweza
kujikuta ndoa yako inakuwa na migogoro isiyokwisha kwa sababu ya kuonekana una
ghubu kwa kujaribu kumbadilisha mwenzi wako na mwisho wake upendo unakuwa haupo
na kisirani katika ndoa kinaongezeka. Kitendo cha kuonekana kuwa na ghubu
kinaweza kumuingiza mwanaume katika tabia nyingine mbaya ya kutotumia muda
mwingi kukaa nyumbani kwake na kutafuta kampani nyingine, kama akipata kampani
ambayo siyo nzuri anaweza kuangikia katika nyumba ndogo ambayo itamkubali bila
masharti.
2.Njoo
tuishi:
Unaweza
kukutana na mwanaume ambaye ana nyumba nzuri au amepanga nyumba nzuri na ana
kila kitu ndani pamoja na usafiri, anakuwa mwepesi kukupa funguo za nyumba yake
ili uhamie muishi pamoja, lakini haweki msimamo wake wazi kwamba ana matarajio
gani na wewe. Kabla ya kukubali kupokea funguo na kuhamia kwake jiulize kama
unampenda kwa dhati au umekubali kwa sababu ya nyumba yake nzuri. Kumbuka
nyumba na vitu vingine vinavyotizamika kwa macho (material things) havina
mashiko linapokuja swala la kupenda. Kupenda kunahusisha vitu vya ndani kama
vile kupenda kwa dhati bila masharti wala kuangalia sifa za nje, kuwa na amani
moyoni kila umwonapo mpenzi wako, kuwa na furaha wakati wote mnapokuwa pamoja,
kupatwa na msisimko wa mapenzi kila umwonapo au usikiapo sauti yake nk. Lakini
kama utamkubali mwanaume kirahisi kwa sababu tu kakukabidhi funguo za nyumba
yake wakati huna mapenzi ya dhati ni janga kubwa kwa sababu hivi vitu vya nje
vinaweza kutoweka kirahisi, sasa je ikitokea si mapenzi nayo yatakuwa
yamekwisha? Kumbuka kwamba kile kilichokupeleka kwake hakipo.
3.Amekuwa
ni liwazo kwako
Liwazo
linaweza kuwa sehemu ya mapenzi lakini hivi vitu haviendi pamoja. Unaweza kuwa
na mwanaume ambaye mnapendana na mnakamilishana hii ni tofauti na mwanaume
unayempenda na ukamgeuza kuwa liwazo pale unapohisi upweke. Jiulize, je ni
kwamba mnapendana na mnafurahi kuwa pamoja au unampenda kiasi kwamba huwezi
kuishi bila uwepo wake. Hapa nazungumzia utegemezi wa kihisia, yaani unakuwa
king’ang’anizi mpaka mwanaume anakuona kero, badala ya kufurahia mahusiano yenu
mwanaume anakuona kuwa ni kero kutokana na kuwa tegemezi wa kihisia. Hakuna
mwanaume anayependa mahusiano ya aina hii anachoka haraka kihisia na
atajitahidi kwa kila namna kukukwepa na ikiwezekana kukutosa na kutafuta
ustaarabu mwingine jambo ambalo litakuumiza sana.
4.Mwanaume
king’ang’anizi:
Mwanaume
kutongoza na kukataliwa siyo jambo linalowashughulisha sana kwao kujaribu na
kukosa ni sehemu ya maisha, lakini lipo suala la kung’ang’ania, yaani mwanaume
kumfuatilia mwanamke kwa hali na mali na kujitoa ili kuhakikisha anampata
mwanamke anayemtaka. Huu ni mtego wa mapenzi, kwani kwa mwanaume kung’ang’ania
na kufuatilia mwanamke kwa muda mrefu bila kuchoka hata asumbuliwe kiasi gani
haimaanishi kwamba mwanaume huyo amempenda mwanamke huyo. Wakati mwingine ni
matamanio tu ndiyo yamemsukuma kutokana na sifa za nje alizo nazo mwanamke
huyo. Kupenda kwa mwanaume kunahusisha zaidi sifa za nje kuliko za ndani na
ndiyo maana mapenzi ya aina hiyo hayadumu yanaanza kama kichaa na kuyeyuka ghafla
kama kipande cha barafu juani. Pale mwanamke anapokutana na mwanaume
king’ang’anizi na asiyekubali jibu la hapana, kabla ya kukubali ajiulize kama
anakubali kuwa na mahusiano na mwanaume huyo kwa sababu amempenda kwa dhati au
kwa sababu ya uking’anga’nizi wake? Kumbuka kwamba wapo baadhi ya wanawake
wanaweza kumkubali mwanaume tu kwa sababu amemfuatilia sana, anajiwa na huruma
anakubali kuwa na mausiano naye siyo kwa sababu amempenda bali kwa sababu ya
huruma. Ni vyema ukajiuliza kama na yeye atathamini huruma yako au akishapata
alichokitaka atakugeuka na kuwa mwiba mchungu kwako? Tafakari na chukua hatua.
5.Baada
ya kupanda mbegu mmea ukachipua
Umekuwa
na uhusiano na mwanaume huyu kwa muda mrefu, lakini hakuwahi kukutamkia kwamba
ana matarajio gani na wewe kuhusiana na swala la ndao, ghafla unakoma kuziona
siku zako… Mimba hiyo! Je unafanyaje?
Kwanza
naomba ufahamu kwamba, kupata mimba haimaanishi ndiyo kuolewa. Hili ni kosa
ambalo wanalifanya wanawake wengi tena wa kiwango cha kutosha, wanaamini kwamba
kubeba mimba kutawahakikishia kuolewa na mwanaume aliyempa ujauzito. Kwa huku
kwetu sheria haziwabani sana wanaume linapokuja swal la kulea mimba na matunzo
ya mtoto kwa hiyo mwanaume kumtosa mwanamke aliyebeba ujauzito siyo jambo la
kushangaza. Wanawake ambao ni single mother wanajua kuhusu jambo hilo. Kwa hiyo
kama unabeba mimba fanya hivyo ukiwa umejiandaa kujitwika changamoto
zitakazojitokeza na usije ukajifariji ukidhani kutakuwa na masaada kutoka kwa
mwenzi wako, utakuwa unajidanganya. Kama akikubali mfunge ndoa sawa, kama
akikubali kulea mimba na mtoto atakeyezaliwa pia ni sawa, akikataa wala
usivunjike moyo, simama imara na songa mbele na maisha kwani kuzaa kabla ya
ndao siyo mwisho wa maisha, yapo maisha tena mazuri sana ukiwa na mwanao. Kwanza
unaye mtu wa kukuliwaza, na pili utakuwa umajihakikishia kwamba wewe si mgumba,
na tatu leo na kesho umekuwa mtu mzima unaye wa kukushika bega kuliko kutegemea
ndugu zako.
6.Pesa
inapokuwa sehemu katika kupenda.
Wapo
baadhi ya wanawake kabla ya kumkubalia mwanaume wanaangalia anamiliki kitu
gani, amesoma kwa kiwango gani, ana kazi ya aina gani, anafanya shughuli gani,
anazo fedha za kutosha au yuko katika mazingira ya utafutaji yanayoashiria
neema huko mbeleni. Sikatai kwamba wanawake kabla ya kumkubali mwanaume
wanataka kujihakikishia usalama, na kama nilivyowahi kusema hapa mara nyingi
kwamba usalama kwa mwanamke maana yake ni mtu kuwa na fedha, tofauti na zama za
kale za mawe ambapo uwindaji na kilimo kilimuweka mwanaume shupavu katika
nyanja hizo kukimbiliwa na wanawake. Siku hizi hayo hayapo, fedha imekuwa ni
njia ya mkato katika kupata kila kitu. Kwa mwanamke fedha ni mtego umnasao kama
panya na kipande cha nguru mtegoni. Siku hizi ukiwa na fedha una uwezo wa
kumpata mwanamke umtakaye, fedha imekuwa kama tufani, inabeba waliomo na
wasiokuwemo, hata wale watakaotokwa na povu kupinga hoja hii, nadhani
hawajapata bahati ya kukutana na wanaume wenye fedha, laiti wangepata
wasingeweza kusimama hapa na kupinga hoja hii. Kwa ushauri tu, si vibaya
kuangalia mwanaume mwenye muelekeo wa kutafuta lakini hicho kisiwe ni kigezo
namba moja, kwani kama akikuonyesha sifa hizo kabla ya kuingia kwenye uhusiano
kisha ukaingia na baadaye ukagundua mwanaume huyo si mali kitu wenyewe mnaita
mwanaume suruale, utaumia sana.
7.
Uzuri wa kitandani
Ninaposema
uzuri wa kitandani namaanisha kuridhishana katika tendo la kujamiiana, kwa
kawaida wanawake ndiyo wahanga wakubwa linapokuja swala la njaa chumbani, wao
ndiyo kwa asilimia kubwa hawaridhishwi na wenzi wao katika tendo. Siyo kwamba
waume zao wana udhaifu, la hasha, inawezekana wanazo nguvu kama za simba,
lakini kwa kawaida tendo la kujamiiana haliwi zuri eti kwa sababu tu mwanaume
anazo nguvu kama za simba, bali inahitaji usanii na utundu ukiwemo werevu wa
kihisia kuweza kumfikisha mwanamke kileleni. Wanaume wengi kwa sababu ya mazoea
wanadhani swala la kumfikisha mwanamke kileleni ni kutwanga kwa kutumia msuli.
Si kweli hata kidogo, ni kumuandaa mwanamke kwa maneno matamu kabla hata ya
kuelekea kitandani. Kwa hiyo wapo wanaume wenye ufundi huo linapokuja swala la
kujamiiana, nia mafundi hodari wenye uwezo wa kuwafikisha wenzi wao peponi,
lakini inawezekana katika maeneo mengine ya kimaisha wakawa watupu kabisa. Siyo
wawajibikaji, wanyanyasaji wakubwa, hawana staha, hawawaheshimu wenzi wao na ni
wenye vurugu kichwani. Wakati mwingine mwanamke anaweza kunasa kwa sababu hiyo
tu, ya ufundi wa kitandani, lakini akajikuta anaishi katika machungu kutokana
na kutothaminiwa na kunyanyaswa kupita kiasi. Kinachomuweka si kingine ni ile
starehe ya muda mfupi wawapo kitandani tu basi. Kuna haja ya kujiuliza, Je ni
kitu gani hasa kinachokufanya umpende mwenzi wako? Kama utamkubali na udhaifu
wake na una uwezo wa kuhimili hizo tabia zisizofaa kwa maana kwamba hazikuumizi
kihisia (kitu ambacho si rahisi sana kwa wanawake) ni sawa, lakini kama huwezi,
sikushauri kuingia katika uhusiano wa aina hiyo, kwani ni kujitafutia kaburi la
mapema.