Umejiandaaje kwa ajili ya siku hiyo? Je, kwako itakuwa siku ya furaha au chanzo cha mateso kwako na kwa mwenzi wako?
Unadhani unatakiwa kufanya nini ili kuifanya siku hiyo kuwa nzuri kwako?
Yapo mengi ya kufanya, lakini kabla ya kuingia huko tuone kwanza maana yake, japo kwa kifupi sana. Marafiki, kuna watu mpaka leo hawafahamu chimbuko na maana halisi ya siku hiyo muhimu. Hapa kwenye All About Love ni mahali sahihi zaidi pa kupata elimu hiyo.
Nini maana yake?
Asili hasa ya siku hiyo ni Roma.
Inaelezwa siku hiyo huadhimishwa kama kumbukumbu ya Padre Valentino ambaye aliuawa na Utawala wa Kirumi uliokuwa chini ya Mfalme Claudia kwa kosa la kutetea waumini wake wafunge ndoa.
Ilivyo ni kwamba, Mtakatifu Valentino alikerwa na Utawala wa Kirumi ambao uliwakataza vijana kufunga ndoa na badala yake kwenda vitani. Kwa msingi huo vijana wakawa na vimada nje hivyo kwenda kinyume na utaribu na maagizo ya imani aliyoisimamia.
Kwa sababu hakupenda hilo liendelee, akaamua kuendesha zoezi la kuwafungisha ndoa vijana kwenye makatakabo (mahandaki chini ya kanisa) kwa siri kubwa.
Hata hivyo, aligunduliwa na kufungwa na baadaye kuhukumiwa kifo. Kwa msingi huo, kwa sababu Mtakatifu Valentino aliuawa siku na tarehe kama hiyo, ikatangazwa rasmi kuandhishwa kwa ajili ya kumkumbuka kama Baba wa Upendo – mtetezi wa wanandoa.
Ikumbukwe kuwa, Padre mwenyewe alikuwa akiitwa Mtakatifu Valentino (unaweza kumuita Valentine), kwa maana hiyo, ilikuwa siku yake – ya kukumbuka alivyopenda watu wapendane.
Awali ilianza kuadhimishwa Roma, lakini baadaye ikaenea katika nchi za Magharibi na dunia nzima kwa jumla. Wakati mapokeo ya kuadhimisha siku hii yalipoanza, ilionekana kama ni ya kidini zaidi, lakini baadaye ilipochunguzwa mantiki ya uadhimishwaji wenyewe, ikaonekana kuwa na maana kwa watu wa madhehebu yote.
Aliyetangaza rasmi kuadhimishwa siku hiyo ni Papa Gelasius, ambapo alisema ikumbukwe kama ishara ya kumuenzi mtetezi wa ndoa, Mtakatifu Valentino.
Iadhimishwe kwa maana yake halisi
Baadhi ya watu wameibadilisha maana ya siku hii muhimu kwa wapendanao. Wenyewe wanahisi kuwa ni siku ya kufanya mambo yasiyofaa. Kwao, wapendanao ni ngono. Kuna ambao huanzisha uhusiano siku hiyo kwa lengo la kupata mtu wa kustarehe naye, hili ni kosa.
Kuna baadhi wamekuwa wakifanya vurugu na kila aina ya uchafu. Si maana yake. Kama nilivyotangulia kusema, ni siku ya kuonyeshana namna mnavyopendana na kuthaminiana. Msingi hasa hapa ni pendo la kweli.
Wewe unaiadhimishaje?
Wewe unaadhimishaje? Huwa una kawaida ya kufanya nini kwa ajili ya siku hiyo muhimu kwa ajili ya penzi lako?
Tunatofautiana kufikiria, kupanga na kufanya mambo.
Inawezekana umezoea kumchukua mpenzi wako na kwenda naye katika hoteli ya kitalii kisha mnakula raha zenu huko halafu sikukuu inakuwa imeisha!
Si vibaya! Labda una mpango wa kushinda na mwenzako ndani siku nzima. Mwingine inawezekana anapanga kwenda katika ukumbi wa burudani na kusikiliza nyimbo nzuri za wapendanao. Si mawazo mabaya.
Hata hivyo, rafiki zangu lazima ufikirie kufanya jambo kubwa, maalum ambalo si tu halitasahaulika bali litatengeneza kitu kikubwa katika historia ya mapenzi yenu.
Inawezekana umeumiza kichwa sana ukijaribu kufikiria kitu cha kufanya kwa ajili ya kunogesha penzi lako, kuifanya ndoa yako kuwa imara, lakini uwezo wako wa kufikiri umefika mwisho na hujapata cha kufanya.
Ngoja nikuambie, umewahi kuwaza kuhusu kufanya hafla ya wapendanao? Hafla ya wapendanao ni nzuri, maana huwakutanisha wenzi na kupanga pamoja namna ya kuishi kwa amani na upendo.
Muda bado unaruhusu, wiki ijayo nitakuwa hapa kukuelekeza namna ya kufanya, USIKOSE!
jocyberspace.. CLICK THE LINK BELOW TO WATCH THE VIDEO ONLY 1.5MB== >